Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, matembezi hayo yaliyofanyika chini ya usimamizi wa Taasisi ya Khatamul Anbiyaa, inayosimamiwa na Alhaji Ghulam Hussein, ambayo imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuandaa shughuli za kidini na kuwakutanisha waumini katika matukio mbalimbali ya Kiislamu.
Katika matembezi hayo, waumini walikusanyika kwa wingi wakiwa wamejawa na huzuni ya kumbukumbu ya siku ambayo Umma wa Kiislamu ulipata pigo kubwa kwa kufariki kwa Mtume Muhammad (saww). Matembezi hayo yalikuwa ni ishara ya mapenzi na uaminifu wao kwa Mtume (saww), huku yakitoa nafasi kwa waumini kutafakari maisha yake, juhudi zake katika kuufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu na mafundisho aliyoyaacha kwa wanadamu.
Jambo lililolifanya tukio hilo kuwa la kipekee ni ushiriki mkubwa wa Wamasai, ambao walijitokeza kwa wingi katika matembezi hayo. Waumini hao wanapatikana katika kijiji cha Mti Mmoja, wilayani Monduli, mkoani Arusha, na walishiriki kwa moyo mmoja katika kuadhimisha kumbukumbu hii muhimu ya historia ya Uislamu.
Ushiriki wa Wamasai katika tukio hilo umeonesha kwa namna ya kuvutia kwamba mapenzi kwa Mtume Muhammad (saww) hayafungwi na kabila, lugha wala mazingira ya mtu; bali yanaweza kuunganisha nyoyo za waumini kutoka jamii mbalimbali chini ya ujumbe mmoja wa imani. Wakiwa katika matembezi hayo, waumini walionesha mshikamano na kuhifadhi kumbukumbu ya Mtume (saww) kwa namna yenye kuleta hisia za huzuni na wakati huo huo kuimarisha umoja.
Kwao, kumbukumbu ya kifo cha Mtume (saww) haikuwa siku ya majonzi pekee, bali ilikuwa pia fursa ya kuhuisha mafundisho yake na kuwakumbusha waumini wajibu wa kushikamana na njia ya haki, maadili, upendo na mshikamano alioufundisha. Kila hatua ya matembezi hayo ilikuwa kama ujumbe kwamba licha ya kupita kwa karne nyingi tangu Mtume (saww) aliporejea kwa Mola wake, nuru ya ujumbe wake bado inaendelea kuangaza katika nyoyo za waumini.








Maoni yako